ujasiriamali Dodoma


UJASIRIAMALI,

Aprili 27, 2012
DODOMA: Ukosefu wa mafunzo ujasiriamali kwa vijana wengi nchini umeonekana kuchangia vijana wengi kuwa tegemezi na wengine  kujiingiza katika ajira zisizo rasmi ili waweze kujikimu.
Kutokana na hali hiyo vijana wengi wamekuwa wakitangatanga na kuzurura huku baadhi yao wakiingiza katika ajira zisizo rasmi ambapo wamekuwa wakijihusisha na biashara haramu za kuuza na kutumia madawa ya kulevya na wakati mwingine hujihusisha na biashara ya ngono.
Baadhi ya vijana wanalazimika kujitumbukiza katika ajira ambazo siyo rasmi na zenye kipato duni kama anavyoeleza Nicolous Machimo, mjasiriamali anayeendesha mradi wa Babalishe katika eneo la Eneo la Makole, Manispaa ya Dodoma.
Machimo anaeleza kuwa eneo lake la mradi huo siyo rasmi na kwamba mamlaka ya manisaa ya Dodoma imekuwa kero kubwa kwa huduma hiyo inayomwingizia kipato na kuondokana na umaskini.
Amesema vijana wengi wamekosa ujuzi na mafunzo ya ujasiriamali na kwamba upatikanaji wa mitaji ni tatizo kubwa kwa vile mikopo inayotolewa na taasisi za fedha huambatana na masharti magumu ikiwemo riba kubwa na ukosefu wa udhamini wa kupata mikopo.
Mghaha wa babalishe anaoendesha Machimo unahudumia wateja kati ya 150 hadi 200 kwa siku, wengi wao ni wanafunzi wa chuo cha biashara Dodoma (CBE).
“Tunatengeneza vyakula kama chips-mayai, ndizi, kuku wa kuchoma na wa kukaanga. Pia tunauza soda za  na vinywaji vingine,”alisema Machimo.
Mghahawa huo ambao umetoa fursa ya ajira kwa vijana 6 ulianza miaka miwili iliyopita na baada ya kuvunjwa banda mgambo wa manispaa ya Dodoma hivi sasa unaendesha huduma zake chini ya mti mkubwa ambapo jiko banifu limetengwa kando kidogo na katikati huduma za mapishi zikiendelea  kwa kukatakata nyanya, vitunguu na viazi.
“Tutakwenda wapi? Tunalazimika kuendesha shughuli zetu hapahapa,”anaeleza Machimo kwa masikitiko.
Ili kuendesha huduma ya chakula kwenye mgahawa huo inalazimu kununua bidhaa mbalimbali vikiwemo viazi kutoka soko kuula Majengo ambapo gunia la viazi hununuliwa kwa shilingi 65,000/- mbali namahitaji mengine kama nyanya, kuku, vitunguu, ndizi na vinywaji.
“Hii kwangu ni kazi halali inaniwezesha kutunza familia yangu, kulipa pango la nyumba, bili ya maji na mahitaji mengine muhimu,” Machimo anasema.
Hata hivyo baadhi ya wafanyakazi wa mghahawa huo wanalalamika kuhusu kipato kidogo kisicholingana na ugumu wa kazi.
Christopher Killian anasema analipa pango shilingi 15,000 kila mwezi, bili ya maji shilingi 3000 na fedha zote zinaishia bila kuona faida ya kazi yake.







Anapendekeza Taasisi za fedha na mamlaka ya manispaa ya Dodoma kuweka utaratibu wa kutambua vijana wajasiriamali wenye mitaji midogo na kuwatafutia njia rahisi za kupata mikopo yenye masharti nafuu na kutoa mafunzo maalum ya ujasiriamali. (Daniel Msangya, Paul Mabeja, Asha Mwakyonde, Noel Stephen, Christopher Mayeye na Joel Mjengi).

Comments

Popular posts from this blog

KIZIGO AWAPONGEZA RUWASA,AKERWA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA,AWATAJA MADIWANI.

HISTORIA YA MPWAPWA HATARINI KUTOWEKA

DC KIZIGO ATOA MAAGIZO KWA KWA MAAFISA ELIMU KUKABILIANA NA UKATILI MASHULENI.