SINA MPANGO NA CHADEMA.
0digg
Dotto Kahindi na Leon BahatiKATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema chama chake hakina mpango wa kuutumia mkutano wake wa leo kwenye Viwanja vya Jangwani kujibizana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na badala yake, kitajikita zaidi katika kutoa somo kwa wajumbe wapya wa mashina na viongozi wa matawi Mkoa wa Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Nape inatoa mtazamo tofauti na tetesi kwamba CCM kitatumia mkutano huo kukijibu chama hicho kikuu cha upinzani ambacho nacho kilifanya mkutano kwenye viwanja hivyo hivi karibuni.
Katika mkutano huo ambao Chadema kilizindua Mpango wake wa Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) mwishoni mwa mwezi uliopita, kiliorodhesha shutuma nyingi dhidi ya Serikali ya CCM zikiwemo za kusababisha maisha magumu kwa Watanzania.
Nape alisema mkutano huo uliandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam hata kabla ya huo wa Chadema na lengo lake ni kuwakutanisha viongozi wapya wa chama hicho tawala na viongozi wa juu wa chama na Serikali, wakiwemo mawaziri watakaofafanua shughuli zao za kiutendaji.
“Mkutano huu unalenga kuwafundisha wajumbe wa nyumba kumi na viongozi wa mashina waliochaguliwa hivi karibuni namna ya utendaji wa Serikali, kwa kuwa wao bado ni wapya kiuongozi na wanahitaji kupewa somo,” alisema Nape.
Alipoulizwa kama mkutano huo ni moja ya hatua za kufuta nyayo za Chadema hasa baada ya kuzindua M4C, Nape alisema: “Mkutano huu tuliuandaa mapema kabla hata ya Chadema hawajafanya mkutano wao. Ila kilichochelewesha ni Mkutano wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM,” alisema Nape na kuongeza:
“Mkutano huu awali, ulikuwa ufanyike ndani ya ukumbi lakini kwa kuwa watu wengi walipenda kushiriki tumeamua kuufanyia Jangwani ambako wanachama na viongozi wa CCM watapata fursa ya kusikia sera za viongozi wa chama na watendaji wa Serikali.”
Aliwataja mawaziri ambao watakuwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ambaye atazungumzia masuala ya usafiri wa reli, bandari na anga na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ambaye atazungumzia masuala ya miundombinu na barabara.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira ambaye atazungumzia hatima ya Watanzania katika masuala ya ajira na vijana na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye atazungumzia mipango ya wizara yake.
Comments
Post a Comment