Jaribio la kumwondoa Papa lanukia Vatican | Send to a friend |
Tuesday, 29 May 2012 21:11 |
VATICAN, Rome TAARIFA za kuvuja kwa nyatraka za siri kutoka ofisi ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani zimeibua taswira mpya, wataalamu wakieleza kuwa zinaambatana na mchakato wa kuanza kumuandaa kiongozi mpya wa Kanisa hilo, atakayechukua nafasi ya kiongozi wa sasa, Papa Benedict XVI. Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya kanisa hilo mjini Vatican, wameeleza kuwa hilo ni jaribio la kwanza la kumwondoa madarakani Papa Benedict XVI. Nyaraka hizo za siri ambazo zimepewa jina la "Vatileaks" zimesababisha kashfa mpya katika kanisa hilo, zikifichua mpango wa kumwondoa madarakani, Tarcisio Bertone, Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican ambaye anaonekana kuwa na sauti na madaraka makubwa, kiasi cha kwenda kinyume na maadili ya kanisa hilo. Huku Vatican ikiendelea kusafisha waovu na wanaovujisha nyaraka hizo kutoka dawati binafsi la Papa Benedict XVI, uvumi umezagaa kwamba mzozo huo unazidi kutanuka na kwa sasa ni vigumu kuuzima. Kanisa Katoliki limekuwa na rekodi mbaya ya kuzima kashfa ambazo zimewahi kulikumba kama vile za utakatishaji fedha, udhalilishaji watoto na kashfa ya sasa inaweza kuanzisha mchakato wa kusaka Papa mpya. "Kundi la makadinali kadhaa katika Vatican limeanza kwa siri mchakato wa kumwondoa Waziri wa Mambo ya Nje, kufikiria pia mchakato wa kusaka mrithi wa Papa (conclave) wakiangalia ni nani anafaa miongoni mwao," limeeleza gazeti La Repubblica la Italia. "Nyaraka hizo zilizovujishwa zinamhusisha Kardinali Bertone kwa njia moja au nyingine," anaeleza Marco Politi, mtaalam wa masuala ya Vatican wakati akizungumza na Shirika la Habari la AFP. "Huu ni mpango wa kumwondoa na kuweka waziri mwingine," ameongeza mtaalam huyo. Bertone, ambaye ni mshirika na rafiki wa karibu wa Papa Benedict XVI, amezusha mijadala mkali hasa kuhusu uendeshaji wa benki ya Vatican, jambo ambalo limetia doa uongozi wa kanisa hilo. Nyaraka hizo zimefichua siri nyingi za Vatican, zikiwamo za matatizo ya ulipaji kodi, udhalilishaji wa kijinsia wa watoto na majadiliano na makundi ya waasi wenye msimamo mkali ndani ya kanisa hilo. Ingawa nyaraka hizo hazitoi habari za kushtua wala kushangaza, zimefungua ‘dirisha la sumu’ ambayo imekuwa ikisambaa miongoni mwa watendaji wa Vatican. Taarifa hizo ambazo zilivuja Januari mwaka huu zinaonyesha kuwapo kwa mzozo mkubwa baina ya Bertone na Askofu Mkuu Carlo Maria Vigano, ambaye amekuwa akijaribu kusafisha hesabu za Vatican, kiasi cha kuondolewa ikidaiwa kwamba ni kutokana na kupambana na maovu. Askofu Vigano alimwandikia barua Papa Benedict na kuomba asiadhibiwe kwa kuondoa waovu na wale waliohusika na matumizi mabaya ya fedha za Vatican ambazo zimesababisha benki inayomilikiwa na kanisa hilo kupoteza mamilioni ya euro kwa kuingia mikataba mibaya, lakini hakufanikiwa. Watu walio karibu na Vatican wanamtuhumu Papa Benedict XVI kwa kutokuwa thabiti na kukosa nguvu za kupingana na uamuzi wa Bertone. "Risasi hizi zinamlenga Bertone. Zinalenga kumwangusha na kumzamisha, kwa lengo la kutaka ajiuzulu," alieleza mtaalam wa theolojia wa Italia, Vito Mancuso akizungumza na wanahabari wiki jana. Kardinali huyo mwenye umri wa miaka 78, pia anatuhumiwa kwa kulazimisha benki ya Vatican kumtimua kazi mkuu wake, Ettore Gotti Tedeschi, ambaye ni mtaalam wa masuala ya fedha kwa kushindwa kufuata maagizo. Gotti Tedeschi alikabidhiwa jukumu la kusafisha Vatican na kuirejesha katika nchi zenye vitabu safi vya hesabu, lakini alishindwa baada ya Bertone kusisitiza kwamba benki hiyo inao uhuru wa kujiendesha, bila kuingiliwa. "Bertone ana madaraka makubwa. Tunatakiwa kuondoa uoza ndani ya kanisa," alieleza mmoja wa maofisa wa Vatican akizungumza na gazeti la La Repubblica. "Wale wanaovuisha siri, wanafanya hivyo kwa maagizo ya papa," kilieleza chanzo hicho. Mzozo huo uliingia sura mpya baada ya Vatican kutishia kumshitaki mwandishi wa habari Gianluigi Nuzzi kwa kitabu chake kipya "His Holiness", ambacho kimeandikwa kwa kutumia nyaraka hizo zilizovujishwa. Kama njia ya kuzuia kuvuja zaidi kwa nyaraka hizo, Msaidizi wa Papa Benedict, Paolo Gabriele amekamatwa kwa tuhuma za kuvujisha nyaraka hizo na amekuwa akihojiwa na watu wengine walioko karibu na Papa. Uvumi umezagaa kuhusu watu 20 ambao wamekuwa wakivujisha siri hizo kwa vyombo vya habari, huku wawili kati yao ambao wamezungumza kwa masharti ya kutotajwa wakieleza kwamba Vatican imechafuka haiwezi kujisafisha. "Kitu dhahiri ni kwamba Tarcisio Bertone hawezi kujiondoa katika kashafa hii kwa sasa," alieleza mtaalamu wa masuala ya Vatican, Sandro Magister. "Hawezi kupona, kuna kila dalili kwamba papa atachukua uamuzi wa kumwondoa na kumweka mwingine katika muda mfupi ujao." Kulingana na mtaalam mwingine, Bruno Bartoloni, siri hizo za "Vatileaks" ni kashfa ambayo inakamilisha miongo ya utawala mbovu na rushwa unaoitesa Vatican. |
Comments
Kwa awamu mbili mfululizo amekuwapo Papa asiyekuwa Italiano.Hiyo ni adha kwa wenyeji.Zengwe la kuvujisha siri ni mpango
kurejesha upapa kwa wenyeji.Hata utakatifu ni nadra kwa mtu mweusi kwa mfano.Mapapa wageni wameondoa ukiritimba wa wenyeji hapo
vatican.Rushwa ni mdudu wa ajabu na hana aibu.Si ajabu kwa hao wapanga mageuzikuwa
wamepewa rushwa ili wachafue hewa hapo.
Dini ya Katoliki imo kwenye taabu ya utovu
wa uadilifu na nidhamu kwa makasisi.Mambo
yasiyofaa yamepatikana kwa viongozi hawa wa Kanisa.Mkatoliki sasa hivi hana la kujivunia isipokuwa imani yake.Angalia msisitizo uliopo kwenye ukusanyaji wa pesa kwa malengo aina aina.Sina hakika na kasi ya uchangishaji huu wa pesa unaendelezaje
maisha ya kiroho ya muamini.Kwa kifupi hii
kasi ya kuongezeka kashfa ndani ya Kanisa
Katoliki,inazid i kuhamisha watu kwenda
dini za kipentekoste.