VIONGOZI YANGA CHAGUENI VIONGOZI BORA
viongozi bora | Send to a friend |
Monday, 09 July 2012 11:26 |
0digg MWISHONI mwa wiki hii utafanyika uchaguzi wa viongozi wa Yanga kwa ajili ya kujaza nafasi zilizo wazi za Kamati ya Utendaji.Uchaguzi huo unafanyika baada ya wajumbe saba wa Kamati ya Utendaji ya Yanga kujiuzulu pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga kujiuzulu pia. Hivi sasa klabu ya Yanga inaongozwa na sekretarieti ya Yanga chini ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo Celestine Mwesigwa mpaka uchaguzi utakapofanyika Julai 15. Uchaguzi wa Yanga utakaofanyika mwishoni mwa wiki utakuwa kwa ajili ya kupata Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe. Wanachama mbalimbali wa Yanga wanaowania nafasi tofauti za uongozi walikuwa wakifanya kampeni katika siku za hivi karibuni, ambapo Jumapili ijayo itakuwa ni siku ya wanachama wa Yanga watakaopiga kura kuchagua viongozi wanaowaona wanastahili kuongoza klabu yao. Tunafahamu kufanya uchaguzi ni gharama hivyo tunaamini wanachama wa Yanga watakaopiga kura mwishoni mwa wiki hawatautumia uchaguzi huo vibaya ila watatautumia kuhakikisha wanapata viongozi sahihi wa kuiongoza klabu yao kubwa nchini. Wanachama wa Yanga wanatakiwa kuchagua viongozi wenye nia ya dhati ya kuisaidia Yanga na siyo kuchagua viongozi wanaotoa fedha kulazimisha kuingia madarakani. Siyo vizuri wanachama wakaangalia fedha na kuwaacha watu muhimu ambao wanaweza kuisaidia Yanga kupata mafanikio makubwa nchini, barani Afrika na duniani. Tunasema hivyo kwa sababu wanachama wa Yanga ndiyo wenye uamuzi hivyo hawatakiwi kufanya makosa na kuchagua viongozi kwa sababu wamepewa fedha ila wanatakiwa kuchagua viongozi ambao watahakikisha Yanga inapata mafanikio. Tunapenda kuwashauri wanachama wa Yanga kukumbuka kuwa kila mara wanapopata nafasi adhimu ya kuchagua viongozi wao wawe wanatumia vizuri nafasi hiyo na kuchagua viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuiletea maendeleo klabu hiyo. Wanachama wa Yanga wanaelewa hawawezi kupata malaika wa kuongoza klabu hiyo kwa kuwa viongozi wao hutoka miongoni mwao wanachama wa Yanga. Tunaamini ili klabu ya Yanga iendelee inahitaji viongozi makini wenye sifa stahiki za kuiongoza klabu hiyo, kama wanachama watachagua viongozi ambao hawana sifa za kuiongoza klabu hiyo wajue watairudisha sana nyuma Yanga na michezo nchini. Uchaguzi wa safari hii wa Yanga ni muhimu labda kuliko chaguzi nyingine zilizopita za Yanga kwa sababu safari hii uchaguzi unafanyika wakati aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga alijiuzulu kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi. Wanachama wa Yanga siku zote ndiyo wamekuwa ngazi ya kuwaweka madarakani viongozi wa klabu hiyo wanaoshindwa kuisaidia timu hiyo na wanaoisaidia timu hiyo ila tunaamini katika uchaguzi huu wanachama wa Yanga watatumia vizuri haki yao ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaostahili kuiongoza Yanga na kuisaidia Yanga. Kwa msingi huo, tunawasihi wapiga kura wa Yanga kutumia busara katika uchaguzi huo wa mwishoni mwa wiki. Tunaamini wakipiga kura zao kwa busara wataleta mapinduzi ya uongozi ambao utaisaidia Yanga. Tunatarajia pia zoezi la kupiga kura litafanyika kwa ufanisi mkubwa na hakutakuwa na udanganyifu wa aina yoyote. Ni matarajio yetu katika uchaguzi wa mwishoni mwa wiki wa Yanga watapatikana viongozi makini ambao watasimamia maendeleo ya Yanga, kwa sababu tunaamini klabu ya Yanga inastahili viongozi bora. |
Comments
Post a Comment