na noel stephen
SERIKALI imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri, maafisa elimu wa mikoa
na wilaya nchini, pamoja na wakuu wa shule, kuhakikisha fedha
zinazotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Camfed linalojihusisha
na masuala ya elimu kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Naibu waziri ofisi
ya waziri mkuu tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Elimu,
Kassim Majaliwa, alisema wizara imejipanga kuongeza juhudi za
ufuatiliaji wa fedha hizo ili kuhakikisha zinawafikia walengwa na
haitasita kuwachukulia hatua kali watakaotumia fedha hizo kinyume.
Alisema serikali tayari imeonyesha jitihada za kudhibiti fedha hizo
ambazo zinafanya kazi ya kuboresha elimu hususan kwa watoto wa kike.
Hata hivyo, alisema baadhi ya walimu wakuu ambao walibainika kuzitumia
fedha hizo kinyume na matakwa walisimamishwa kazi na wengine kushushwa
vyeo.
“Kwa mfano kwa aliyekuwa mwalimu mkuu wa nyamisati na mwenzie wa
kibiti tuligundua maeneo ambayo mtoto anapaswa kupewa fedha kwa ajili
ya mahitaji mengine lakini walimu hao walikuwa hawatoi,”alisema
Aidha, Naibu huyo, alisema tayari serikali imeweka mazingira mazuri
ili Camfed iweze kufanya kazi kwa umakini na usahihi katika kuiboresha
sekta ya elimu nchini.
Alitoa wito kwa taasisi mbalimbali na mashirika yasiyo ya kiserikali
yanayojihusuisha na elimu kutatua changamoto zilizopo kwa kushirikiana
na serikali.
“Camfed ni miongoni mwa taasisi zilizoingia kwa vitendo na imeshiriki
kikamilifu katika kutatua changamoto zilizopo,”alisema
Kwa upande wake Naibu waziri wa Tamisemi anayeshughukia serikali za
mitaa, Aggrey Mwanri, alilihakikishia shirika hilo kupata ushirikiano
wa kutosha kutoka katika wizara hiyo ili kuhakikisha walengwa
wananufaika na ufadhili huo.
Alisema katika hali ya kawaida shughuli hiyo ilipaswa ifanywe na
serikali lakini kutokana na jitihada za shirika hilo serikali
itaungana nalo ili kufikia malengo yake.
Alifafanua kuwa tayari shirika hilo limeshatumia bilioni tisa, kwakuwa
sasa watafanya kazi pamoja atahakikisha fedha hizo zinawafikia
walengwa.
Naye mkurugenzi wa shirika hilo nchini, Msaada Daudi Balula, alisema
shirika hilo makao makuu yake ni Cambridge uingereza ambalo mkurugenzi
muasisi wa shirika hilo ni Ann Cotton ambaye alianza kwa madhumuni ya
kusaidia watoto wa kike kupata elimu na kujipatia ajira.
Alisema shirika hilo limeweza kusaidia watoto 6,332 tangu mwaka 2005
kupitia mradi wa Bursary na watoto 64,227 kupitia mfuko wa dharura.
Alisema pia kumekuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na
tatizo la utoro na mimba kwa wafadhiliwa, kukosa ushirikiano kwa
wanajamii, ufaulu mdogo, na matumizi mabaya ya fedha za wafadhiliwa
yanayofanywa na baadhi ya wakuu wa shule.
a
Shirika hilo linafanya kazi katika wilaya za Bagamoyo, Iringa
vijijini, Morogoro vijijini, Handeni, Pangani, Kilombero, Kilosa,
Kibaha, Kilolo na Rufiji.
Mwisho.
Comments
Post a Comment