STARS WAFIKA ABJANI HOI


0digg
Mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samata akiwa amelala kwa uchovu katika viti kwenye uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi wakati wakisubiri kubadilisha ndege kuelekea jijini Abidjan, Ivory Coast. Picha na Edo Kumwembe.
Edo Kumwembe, Abidjan
TIMU ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imetua salama jijini Abidjan jana saa 12 jioni bila ya kiungo wake wa Haruna Moshi 'Boban' aliyeachwa Dar es Salaam kwa madai ya kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.

Hadi juzi wakati kikosi cha mwisho kinatangazwa kulikuwa hakuna taarifa yoyote ya kuumia kwa Haruna mbali ya Nurdin Bakari na Thomas Ulimwengu walioenguliwa mapema kutokana na kuwa majeruhi.

Kocha Kim Poulsen aliiambia Mwananchi jijini Nairobi jana kuwa Moshi 'Boban' hakusafiri na timu baada ya kuumia nyama za paja akiwa mazoezini mara baada ya mechi dhidi ya Malawi.

Poulsen alisema kuachwa kwa Haruna ni pengo kwa kikosi chake, lakini atapata jibu la mchezaji anayeweza kuziba nafasi hiyo baada ya mazoezi ya siku mbili jijini Abidjan.

“Ngoja kwanza niwaangalie wachezaji kwa mazoezi ya hizi siku mbili nitajua nini cha kufanya. Haruna Boban alikuwa katika mipango yangu na ndio maana nilimchezesha katika pambano dhidi ya Malawi, lakini sasa ameumia inabidi niangalie nini cha kufanya,” alisema Poulsen.

Wakati Poulsen akitoa sababu ya kuachwa kwa Haruna kwenye safari hiyo kuwa ni majeruhi, jana mmoja wa viongozi wa Stars alipoulizwa na Mwananchi kwa nini Haruna hakuwapo wakati timu ilipokuwa ikiagwa alisema kuna vitu anafutilia.

"Haruna ameambiwa afutilie vitu fulani na baadaye atajiunga na wenzake tayari kwa safari hiyo," alisema kiongozi huyo bila ya kufafanua ni vitu gani anavyofutilia.

Hivi karibuni gazeti hili liliripoti kuwa kiungo huyo wakati akisindikiza mwili wa marehemu wa aliyekuwa mchezaji wa Simba, Patrick Mafisango  nchini DR Congo alizuiwa kwa muda kuingia nchini humo kutokana na kuonyesha pasi kusafiri ya muda inayotumika kwa nchi za Afrika Mashariki.

Wakati huohuo;Timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' iliwasili jijini Abidjan jana saa 12 jioni baada ya kuganda kwenye Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta wa Nairobi kwa zaidi ya saa tano kufuatia kusogezwa mbele kwa ratiba ya ndege yao ya kwenda Ivory Coast.

Stars iliwasili Nairobi saa 12 asubuhi na ilitazamiwa kuondoka saa mbili asubuhi kwenda Abidjan, lakini ndege waliyotegemea kuondoka nayo ikaharishwa mpaka saa tano asubuhi hali iliyowafanya wachezaji wa timu hiyo watazamiwe kukosa mazoezi ya jioni jijini Abidjan kama ilivyopangwa na kocha Kim Poulsen.

Akizungumzia kitendo cha uwezekano wa kukosa mazoezi ya jana jioni jijini Abidjan, kocha Poulsen alisema hakitaathiri timu yake kwa kuwa wamefanya mazoezi kwa zaidi ya wiki mbili sasa pamoja pia wamecheza mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi Jumamosi iliyopita.

“Pamoja na kutofanya mazoezi bado hakuna madhara kwa sababu tumefanya mazoezi ya kutosha mpaka sasa. Kumbuka pia kuwa tumecheza mechi ya kirafiki kwa hiyo kukosa mazoezi kwa jioni moja sio tatizo,”alisema Poulsen.

Mbali ya wachezaji na benchi zima la ufundi, wengine walioganda kwenye uwanja wa Jomo Kenyatta, Nairobi  ni pamoja na kiongozi wa msafara, Crestencius Magori, Mwanasheria wa TFF, Alex Mgongolwa, Mwenyekiti wa soka la Vijana TFF, Msafiri Mgoyi na Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari za michezo, TASWA, Juma Pinto.

Stars inatazamiwa kujitupa uwanjani dhidi ya Ivory Coast kesho jioni katika pambano la kuwania kufuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 yatakayofanyika Brazil. Mechi nyingine ya kundi hilo itakayochezwa kesho pia itakuwa kati ya Gambia na Morocco itakayochezwa nchini Gambia.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!



7000 symbols left


Banner
Banner

Comments

Popular posts from this blog

DC KIZIGO ATOA MAAGIZO KWA KWA MAAFISA ELIMU KUKABILIANA NA UKATILI MASHULENI.

HISTORIA YA MPWAPWA HATARINI KUTOWEKA

KIZIGO AWAPONGEZA RUWASA,AKERWA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA,AWATAJA MADIWANI.